Simba imeilazimisha Mbeya City sare ya kufungana magoli 2-2 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa taifa.
Mbeya City walianza kupata goli la kuongoza kipindi cha kwanza lililofungwa na Ditram Nchimbi dakika ya 37 kipindi cha kwanza baada ya kuachia shuti kali kufatia kupokea pasi ya kisigino ya Raphael Daudi.
Ibrahim Ajib aliisawazishia Simba dakika ya 65 kipindi cha pili kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya Mohamed Ibrahim kuangushwa nje kidogo ya box la penati. Ajibu aliuchinja mpiara na kuukwamisha kwenye nyavu huku golikipa wa Mbeya City Owen Chaima akiruka bila mafanikio.
Mbeya City hawakukata tamaa, dakika 75 Kenny Ally akaifungia Mbeya City bao la pili baada ya kugongeana pasi na Raphael Breyson ambaye alipiga pasi kwa Ditram Nchimbi aliyepiga pasi ya mwisho kwa Kenny Ally na kukwamisha mpira kambani.
Dakika zikiwa zimeyoyoma Simba wakapata goli la kusawazisha kwa mkwaju wa penati kufatia beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuangushwa kwenye box. Mkwaju wa penati ukapigwa na Shiza Ramadhani Kichuya na kuamua game hiyo kumalizika kwa sare ya kufungana 2-2.
Sare ya leo imeifanya Simba kuongeza pointi moja na kufikisha pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, ipo mbele kwa pointi tatu dhidi ya Yanga yenye pointi 52 lakini inamchezo mmoja ambao itacheza kesho Jumapili February 4, 2017 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Endapo Yanga watashinda mchezo wao wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar, watafikisha pointi 55 sawa na Simba na wataongoza ligi kwa tofauti ya wastani wa magoli dhidi ya Simba.
Simba ni mara ya pili inapata matokeo ya sare ya kufungana 2-2 dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa taifa, mara ya mwisho kupata matokeo kama hayo ilikuwa ni September 21, 2013.
Post a Comment